Friday, January 4, 2013

NAKERWA NA TABIA ZA BAADHI YA WANAWAKE KUZUSHA UGOMVI KWENYE SHUGHULI ZA WATU


Siku ya jumatano ya tarehe 2/01/2013, mimi bibi yenu nilipata mwaliko wa kuhudhuria shuguli ya Kitchen Party ya Mjukuu wa rafiki yangu mmoja ambaye tulikuwa tukifanya nae kazi zamani lakini tayari yeye mwenzangu ameshastaafu kazi miaka miwili iliyopita.
Hivyo, baada ya kutoka kazini, nilirudi nyumbani nikajiandaa na kumuaga babu yenu kisha nikaita usafiri wa bajaji mie huyoo nikaelekea kunako shughuli hiyo. Nilifika ukumbini mnamo saa kumi na moja jioni. Niliingia na kuelekea moja kwa moja sehemu maalum iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya kukaa wazazi. Niliingia na kigelegele kikali ambacho kilimuinua shoga yangu pamoja ndugu wengine wakaribu yake wakaja kunilaki huku wakipiga vigelegele kwa furaha. Shangwe ikalipuka. Niliketi pembeni ya shoga yangu na kuangalia wanawake walivyokuwa wakijimwayamwaya kwa Muziki uliokuwa ukipigwa ukumbini humo. Kila mmoja ukumbini mle alionekana ni mwenye furaha. Bibi harusi alikuwa hajaingia bado. Basi tuliendelea kubadilishana mawazo na kucheza muziki hadi muda wa bibi harusi kuingia ukumbini ulipowadia. Wageni waalikwa wote tulisimama na kushuhudia bibi harusi mtarajiwa akiingia ukumbini. Ukumbi ulilipuka kwa nderemo na vifijo. Ama kwa hakika binti alipendeza hasa.
Basi shugli yetu ikaanza rasmi. Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi alitufungulia rasmi sherehe yetu kisha ratiba moja baada ya nyingine zikafuata. Hatimaye muda wa bibi harusi kufungua Muziki uliwadia. Bibi harusi mtarajiwa alifungua Muziki kisha waalikwa tukapata nafasi ya kujimwayamwaya ukumbini mle.
Wakati Muziki ukiwa umekolea, ghafla tukasikia makelele ukumbini mle. Mabinti wawili walikua wakirushiana maneno makali ya nguoni. Hali ya hewa ilibadilika ghafla ukumbini mle. Na kabla hatujafanya lolote maana tulikuwa tumepigwa na butwaa, mabinti walishikana na kuanza kupigana live.Ukumbi wa sherehe ukageuka kuwa uwanja wa ngumi. Makubwa jamani.
Ilibidi kutumia nguvu ya ziada ili kuwatenganisha na kuwatoa nje kwa nguvu.
"Mjinga wewe, kazi kutembea na wanaume wa wenzako tu, una bahati sana, leo nilikuwa nakuharibu hiyo reception yako, tena nakwambia ugomvi haujaisha bado, ni lazima nikuonyeshe". Aliloloma mmoja wa mabinti waliokuwa wakipigana huku akitweta mithili ya Simba aliyejeruhiwa.
"Kwenda zako mpumbavu wewe, wewe mwenyewe mwizi, mwanaume sio wako. Kila mmoja anakula kwa wakati wake bwana. Na nakwambia hivi, mwanaume wako simwachi ng'o!". Binti wa pili alijibu mapigo. Basi ilizuka tafrani ya nguvu ukumbini. Wamama wenye nguvu zao walifanikiwa kuwatoa kabisa nje ya eneo la ukumbi mabinti wale na waalikwa wakarudi kurudi ukumbini kuendelea na sherehe. Kilichoendelea kwa mabinti wale huko nje mimi na wewe hatukijui.
Kusema ukweli mimi bibi yenu roho yangu ilinichafuka hivyo niliamua kuondoka na hasa ukizingatia kuwa, matukio muhimu yalikuwa yamekwishakamilika. Wapo waalikwa wengine wasiopenda vurugu kama mimi nao waliamua kujiondokea zao.Shughuli ikawa imeharibika.Nilifika nyumbani na kuona ipo haja ya kuongea na wajukuu zangu wa kike kuhusiana na tabia hii mbaya. Nilishika kalamu na kuandika kama ifuatavyo.
Kwenu Wajukuu zangu wa kike,
Ni matumaini yangu kwamba, nyote mu wazima wa afya njema. Mimi bibi yenu sijambo. Babu yenu hajambo pia, anawasalimia sana.
Lengo hasa la barua hii ya leo, ni kuwacharaza wajukuu zangu wa kike ambao wanatabia ya kuzusha vurumai zisizokuwa na maana kwenye shughuli za watu eti kwa sabau ya wivu wa kimapenzi. Tena wapo ambao wao popote watakapokutana basi huzusha ugomvi. Iwe harusini, msibani na hata sokoni jamani. Hivi mmerogwa? Hivi kweli mtu una akili zako timamu kabisa unathubutu kuzusha ugomvi harusini, msibani? Kisa? Mnagombea mwanaume. Kusema ukweli, mimi bibi yenu mnanichafua hasa. Roho yangu inanichafuka jamani.
Halafu ukikaa chini ukawachunguza hao wanaogombana, mara zote fanya utafiti mimi nawaambia,utagundua kwamba, wote wawili hakuna ambaye ni mke halali wa huyo wanayemgombania. Wote ni wezi. Mwenye mume yupo nyumbani ametulia tuli kama maji ya mtungi, nyie wenzangu na mimi huku mnauana. Acheni tabia hiyo wajukuu zangu. Mnatudharaulisha na kututukananisha sisi mama na bibi zenu.
Pengine tu niwaelezeni kwamba, ukewenza haujaanza leo. Na wala nyinyi sio wa kwanza. Enzi zile sisi tunakua, mtu alikua anaweza kutembea na mume wa mpangaji mwenzie ambaye vyumba vyao vinatazama lakini kamwe anayeibiwa hakuweza kugundua kwani muibaji alimuheshimu mke halali na waliweza kuombana mboga kwenye vibakuli, chumvi na hata kuazimana khanga. Sasa ninyi mabinti wa siku hizi mmekuaje? Nasema jirekebisheni. Tabia ya kuzusha vurugu kwenye shughuli za watu mziache. Kama mna nguvu kweli, si mwende mashambani mkalime? Mnajidhalilisha, mnatudhalilisha sisi wazazi wenu na pia mnashusha hadhi zenu. Mnatukanana matusi ya nguoni, mnachaniana nguo, ili iweje? Mnawapa watu sinema ya bure.
Naandika kwa uchungu, hasira zimenibana kweli, hivyo naona niishie hapa kwa leo kwa sababu nikiendelea, mwisho nitawasemea maneno mabaya bure. Mwaka huu wa 2013, mmbadilike.
Ni mimi bibi yenu,
Thereza.
 
 

No comments:

Post a Comment