DAAH!ILIKUWA NI LOVELY COUPLE JAMANI.


Kwako Mjukuu wangu Wastara Juma,
Pokea salamu nyingi za pole kutoka kwangu mimi bibi yako Thereza. Babu yako anakupa pole pia. Ama kwa hakika, sote wawili( mimi na babu yako) tumepokea habari za kifo cha mumeo kwa masikitiko makubwa. Amini usiamini mjukuu wangu, naandika barua hii huku machozi yakinibubujika kama maji hasa ukizingatia kwamba, siku ya jumatatu ya tarehe 31 desemba, 2012 mimi na babu yako tulikua tukiangalia mahojiano yenu (wewe na mumeo) katika kipindi cha mkasi cha EA TV mida ya saa tatu na nusu hadi saa nne usiku. Kusema ukweli, tulifarijika sana kuwaona katika mahojiano hayo kwani wewe na mumeo mlikua mmependeza sana na afya ya Sajuki ilionekana kuimarika tofauti na ilivyokua awali. Vilevile, nyuso zenu zilikua zimepambwa kwa tabasamu wakati wote na mlionekana kuwa na matumaini makubwa. Lakini ghafla mambo yamebadilika. Sajuki ametutoka, hatunaye tena duniani. Pole sana mjukuu wangu Wastara. Mtumaini Mungu katika kipindi hiki kigumu ulichonacho sasa. Rejea hadithi ya Ayubu katika Biblia, ama kwa hakika itakutia nguvu.
Pamoja na hayo, naomba nikueleze kwamba, katika ndoa za Wajukuu zangu zooote, iwe ni kwa wasanii ( Muziki, filamu na fani zingine za sanaa), na wajukuu zangu wengine ambao si wasanii, ama kwa hakika ndoa yako imeshika namba moja. Umeonyesha uvumilivu wa hali ya juu kwenye ndoa yako pamoja na misukosuko yote mliyoipitia wewe na mumeo. Mlishikamana wala hamkutupana. Kila mmoja alipopata shida, mmoja wenu alisimama kwa ajili ya mwenzake. Nakupa pongezi nyingi sana kwani hukunitia aibu mimi bibi yako.
Kupitia ndoa ya Sajuki na Wastara, nawataka wajukuu zangu woote mlio katika mahusiano muige mfano wa mapenzi ya Sajuki na Wastara ili kutujengea heshima sisi wazazi wenu. Maisha ya mahusiano hujengwa kwa upendo wa dhati, kuheshimiana na kuvumiliana. Mkiyashika haya, kwa hakika mtaishi maisha marefu kama ya mimi na babu yenu ambao tumekua katika maisha ya ndoa kwa miaka thelathini na nane. Tumevuka milima na mabonde pamoja hadi leo hii. Nataka nanyi mzeeke pamoja. Sio mwenzio akipata shida kidogo wewe unamkimbia na kwenda kutafuta mwingine. MARUFUKU KABISA.
Naomba nimalizie barua yangu kwa kukueleza Wastara kwamba, tupo pamoja na wewe katika kipindi hiki kigumu. Mimi na babu yako tunakuombea kwa Mungu akutie nguvu ili uweze kuendelea na maisha kwani maisha ni lazima yaendelee mjukuu wangu.
Pokea salamu za pole kutoka kwa babu yako.
Ni mimi bibi yako,
Thereza.