Wednesday, February 20, 2013

WANAWAKE TUSIKWEPE MAJUKUMU YETU YA NYUMBANI

Habari zenu wajukuu zangu. Poleni ni mihangaiko ya kila siku ya kujitafutia riziki. Mimi bibi yenu ni buheri kabisa wa afya njema. Namshukuru Mwenyezi Mungu siumwi hata mafua.
 
Leo nataka niongee na Wajukuu zangu wa kike wale walio kwenye ndoa. Lengo kuu likiwa ni kuwakumbusha majukumu yao wao kama ma mama wa familia. Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wanaume wengi kuwa, Wake zao wamekuwa ni wavivu na hawatekelezi majukumu yao kama ilivyokuwa awali hasa wakati wa uchumba ama mwanzoni mwa ndoa zao.
 
Wajuu zangu, fanyeni mfanyayo lakini mkumbuke kuwa, ninyi ndio mnatakiwa mjue masuala ya usafi wa nyumba, masuala ya chakula, kuhakikisha watoto wanakwenda shule wakiwa safi hali kadhalika, kuhakikisha mumeo anakwenda kazini akiwa smart. Eeh!Nimetia kizungu kuonyesha msisitizo.
 
Naelewa fika kwamba, siku hizi hali ya maisha imekua juu. Bei za vitu zipo juu. Zama tulizonazo leo, sio zile za kwetu za kununu Mkate shilingi 25, Sembe shilingi 75 na nauli ya daladala shilingi moja. Zama hizo zimeshakuwa ni historia. Hivyo kutokana na hali ya maisha kupanda sana, hivi sasa, si mwanamke, si mwanamke, wote tumekuwa ni watafutaji. Hakuna mwanamke anayebaki nyumbani akimsubiri mumewe amletee mchele, sukari, dagaa, chumvi na kiberiti. Mtindo wa sasa ni mwanamme akileta unga, mama naye analeta chumvi, siku zinakwenda. Akina mama tumekuwa ni Wajasiliamali hasa. Wenye kufungua salon wapo tele, sijui akina mama ntilie, Wauza samaki, Wasusi ili mradi tu, kila mmoja anapigana kupata riziki.
 
Lakini, pamoja na hayo yooooote, mimi sitaki hayo yawe ndio sababu ya ninyi kukwepa majukumu yenu ya nyumbani kama ma mama wa familia.
 
Unakuta mwanamke anaamka asubuhi pamoja na mumewe, maji ya kuoga yameshaandaliwa na housegirl, yeye na mumewe wanakwenda kuoga. Haya, chai tayari ipo mezani, imeandaliwa na housegirl, anakunywa na mumewe. Yaani mwanamke hajui watoto wamekwenda shule saa ngapi, wamevaaje, iiiiii, yeye mradi housegirl yupo na anamlipa mshahara basi.
 
Haya, mmekwenda kwenye mihangaiko yenu ya mchana kutwa. Jioni inafika, mnarudi nyumbani. Baba na mama wote mnakikutia chakula mezani. Mmh!Hebu nikuulize wewe mama, hivi, kwa mfano umeketi mezani, chakula ndio kimeshatengwa na housegirl, baba anapakua chakula na kukitia mdomoni kisha anagundua kuwa chakula hicho ni kibichi, kimeungua au hakina chumvi wewe kama ni mwanamke hasa uliyekamilika, utajisikiaje? Hiyo ni aibu kubwa sana kwako wewe.
 
Ombi langu kwenu ninyi akina mama hasa waolewaji, pamoja na kwamba mnamajukumu mengi, lakini, unashindwa nini kurudi nyumbani, ukaenda kuweka mkoba wako chumbani kisha ukaenda jikoni kuangalia chakula kilichopikwa na housegirl na kujiridhisha kama kipo sawa ili kama hakipo sawa, ufanye utaratibu haraka wa kuandaa chakula cha mumeo. Lakini pia si vibaya wewe kama mama kuandaa chakula cha mumeo mezani na kumkaribisha mumeo mezani. Hiyo itamfariji sana mumeo na kujisikia kwamba ana mke ambaye anampenda na kumjali pia. Lakini nawe ukakae tu usubiri housegirl aandae meza kisha awakaribishe wewe na mumeo mezani kwa kweli inashusha nafasi ya mwanamke katika nyumba.
Bibie, housegirl akipika, wewe andaa meza, akifua, wewe piga pasi na kuhakikisha nguo ya mumeo ipo sawasawa au vipi?. Aidha, weka utaratibu wa kuwaona watoto wako asubuhi kabla hawajatoka kwenda shule ili kujiridhisha wapo safi na wamevaa nguo safi tayari kwa kwenda shule. Eee!Maana huwa tunawaona njiani watoto wanakwenda shule wachafu. Hawajaoga, nguo chafu, viatu havieleweki yaani wapowapo tu. Na ukiwaangalia watoto hao na kuwafananisha na wazazi wao, mmh!hawafanani kabisa. Hata kama umewanunulia sare nzuri, viatu vizuri lakini kama nguo hazijafuliwa, hazijanyoosha, viatu havijasafishwa, umaridadi utatoka wapi?
 
Jitumeni Wajukuu zangu kwani mumeo akiwa rafu na watoto wakiwa wachafu, aibu ni yako wewe mama na inaonekana umeshindwa kutekeleza wajibu wako kisa, upo busy. Hapana, busy ya kutafuta riziki tuwe nazo lakini pia, majukumu yetu tuyatimize kwa faida ya familia zetu. Mwanamke ni pambo la nyumba bwana hivyo, sio ujipambe wewe tu ukasahau mumeo na watoto wako. Jitumeni hasa ili kuboresha nyumba zenu na mahusiano kwa waume zenu ili wasijehisi kama walikosea kuwachagua. Mimi bibi yenu najituma, sina mchezo kabisa nyumbani kwangu na ndio maana hadi leo hii, bado ningali nipo na babu yenu.
 
Kwa leo, yangu ni hayo, naomba niishie hapa.
Ni mimi bibi yenu,
Thereza.