Friday, July 19, 2013

KUKOPA SIO DHAMBI WAJUU ZANGU

                        Daima mbele mama


Sinta mjukuu wangu siku zote yanapoinuka mafanikio, vikwazo navyo huinuka. Usijali we fanya yako mama. Kukopa sio dhambi.

Ama kweli, binadamu hawana wema na kwa hakika mtu huwezi ukafanya jambo ukamfurahisha mwanadamu. Siku ngapi hizi mimi bibi yenu nilikuwa nimetulia na fimbo yangu haijachapa mtu kwa muda mrefu lakini kwa hili, aah!aah! nimejikuta nashindwa kujizuia na kuchukua bakora yangu ili niwacaharaze kisawasawa wale wote wenye tabia kama hii ili wajifunze.
Kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kudharau wenzao na kuwakashifu kuwa wana maisha ya hali ya chini na wao kujiona kuwa wapo matawi ya juu. Sawa, kama Mwenyezi Mungu akujalia wewe maisha bora, ni heri na Mshukuru sana kwa hilo na waombee wote walio katika hali duni siku moja Mwenyezi Mungu nao awajaalie. Lakini usitumie umasikini wa mtu kama fimbo ya kumchapia kwani kumbuka kuwa aliyekupa wewe ndie aliyemnyima yeye na dunia ni duara ipo siku unayemdharau atapanda juu na wewe ukashuka chini. Mmh!Hapo sasa. 
Mwanadada wa watu mlikuwa mkizonga kuwa ooh! anaishi maisha ya chini kwani anaishi uswahilini, gari lake ni la bei nafuu sijui kiberiti, mara ooh!ni mzee, hivi hebu kwanza niwaulize, kuwa mzee ni dhambi? Na ni nani ambaye atabaki kijana milele? Nawaambieni nyoote hata muwe na urembo wa kiasi gani, kuzeeka ni lazima. Tena kwanza kuzeeka kwa sasa ni bahati. Vijana wengi wanakufa wakingali wadogo.
Nikirudi kwa upande wa ridhiki, kila mtu hupata kwa wakati wake na imepangwa kwa mafungu, leo kwako na kesho kwa mwenzako. Na pia, si kwamba ukipata basi ndio iwe matangazo dunia nzima. Mwanamke mwenye stara hufanya mambo yake kimyakimya na watu hubaki kujionea wenyewe.
Mlimsema mjukuu wangu sana kwamba maisha yake ni ya chini kumbe hamkujua kuwa mjini mipango na kila mtu na kichwa chake, dada wa watu kajipanga kafungua duka lake tena kwa suprise, mmeibuka eti ooh!kafungua kwa fedha za mkopo mmh!Kweli binadamu hawana jema na siku zote hupenda kuona wenzao wapo chini na wao peke yao ndio wawe juu. Lakini wanasahau kuwa mgawa ridhiki ni allah pekee. Hivi aliyewaambia kuchukua mkopo ni dhambi nani? Kwanza mtu ukipewa mkopo ujuwe wewe upo juu na unaaminika kwani mkopo hautolewi hovyo hovyo tu kwa kila anayeomba katika mabenki. Vipo vigezo ambazo vinaangaliwa ili mtu upate mkopo. Kama ni rahisi hebu kajaribu na wewe uone kama utapewa. Na halafu dunia ya leo, kila mmoja anakopa. Kula yetu, lala yetu na hata biashara zetu, mitaji ya wengi imepatikana kwa njia ya mkopo.
Kwahiyo mjukuu wangu, kama umekopa, au hukukopa wewe fanya yako na waache wao povu la mdomo liwatoke. Nchi yenyewe inakopa au wao hawalijui hilo sembuse wewe? Bibi fanya yako wee! Kopa, ukiona hautoshi kopa tena kadri uwezavyo kikubwa unalipa deni lako.Kwani mabenki, Mabaypot, sijui black na mapride yameletwa kwa ajili gani? Yameleletwa ili kuinua wananchi hasa sisi akina mama. Mimi mwenyewe bibi yako kibanda changu nimejenga kwa fedha ya mkopo halikadharika ada za wanangu.
Na sasa bakora inahamia kwa watumishi wote ambao wanatabia ya kutoa siri za ofisi wanazofanyia kazi kwa manufaa yao binafsi. Mtumishi anayejua vema maadili ya kazi yake kamwe hawezi kutoa siri za ofisi hasa za wateja wa ofisi anayofanyia kazi kwani ni kosa sana. Lakini hili liwe funzo kwa waajiri kuwa makini na watumishi wanaowaajiri katika makampuni yao kwani wengi wao sasa hawana maadili ya kazi. Kwa mtu anayeyajua vema maadili ya kazi yake, na ameapishwa, sijui kama makampuni mengine hasa binafsi yanafanya hivyo lakini kwa sisi watumishi wa umma tunaapishwa na ikigundulika mtu ametoa siri za ofisi hatua kali za kinidhamu huchukuliwa dhidi yake. Hivyo mtumishi atakayebainika kutoa taarifa za kiofisi za mwanadada inayesemekana alikopa katika kampuni fulani achukuliwe hatua za kisheria kwani amemdhalilisha mteja na ofisi yake.