Mmh! Ama kweli ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni. Na wala wahenga wetu hawakukosea kusema hivi.
Ninalazimika kuanza makala yangu ya leo kwa msemo huo baada ya kusimuliwa mkasa na mjukuu wangu mmoja ambao ndio ulionifanya niandike makala hii.
Jana usiku mida ya saa tano hivi za usiku nikiwa nimejipumzisha, kilongalonga changu kiliita. Kusema ukweli, moyo wangu ulishtuka kwa sababu simu za usiku bwana mara nyingi huwa zinaleta taarifa mbaya (msiba, maradhi n.k).
Kabla ya kuipokea, niligeuka kumwangalia babu yenu aliyekuwa amelala pembeni yangu, maskini ya Mungu alikuwa amelala anajikoromea tu hana hata habari. Si unajua usingizi wa uzee tena. Basi sikuona haja ya kumwamsha niliamua nimwache niipokee tu hiyo simu kama itakuwa na taarifa ambayo itabidi nimtaarifu basi nitamwamsha. Nilijikaza na kuichukua simu yangu na kutazama screen ya simu hiyo kwanza kabla sijaipokea.
"Ni namba ngeni". Nilijikuta natamka mwenyewe mara baada ya kuona namba ambayo siifahamu. Wakati bado najiuliza namba hiyo ni ya nani, simu ile ilikata. Lakini kabla sijafanya lolote, simu ile iliita tena. Niliamua kuipokea pasipokupoteza muda.
"Hallow!"
"Hallow!". Ilisikika sauti kutoka upande wa pili. Ilikuwa ni sauti ya kike.
"Habari yako?". Nilimuuliza
"Nzuri. Sijui wewe ni bibi Thereza?'. Aliniuliza
"Ndiye mimi".
"Shikamoo bibi". Aliniamkia.
"Marahabaa, enhee!Nikusaidie nini mjukuu wangu, kulikoni usiku?".
"Samahani bibi kwa kukupigia simu usiku lakini ninatatizo ambalo limenifanya nishindwe kuvumilia hadi asubuhi ifike ndio nikupigie".
"Eeeh!Pole sana mjukuu wangu, ila hujaniambia unaitwa nani".
"Naitwa Mariam".
"Enhee tatizo hasa ni nini mjukuu wangu au umegombana na babu?". Nilimuuliza kwa dhihaka.
"Yaani bibi, bora hata ningegombana na babu yako kuliko hili tatizo lililonifika".
"Ok, hebu nieleze ili nione nakusaidiaje".
Basi Wajukuu zangu Mariamu alinieleza kuwa, yeye kwao walizaliwa watoto watatu, wote wakiwa ni wakike na yeye ndiye mkubwa. Lakini kwa bahati mbaya wazazi wao wote wawili walifariki wakati yeye akiwa kidato cha sita, na mdogo wake mmoja alikuwa darasa la nne na wa mwisho alikuwa darasa kwanza.
Mariamu aliendelea kusema kuwa, baada ya vifo vya wazazi wao, maisha yalikuwa ni magumu sana kwa upande wao kwani waliishi maisha ya tabu sana huku yeye akilazimika kuwa mlezi wa familia. Ajue wadogo zake wanakula nini, wanavaa nini na wakiumwa wanatibiwaje. Chakumshukuru Mungu ni kwamba wazazi wao waliwaachia nyumba hivyo kazi yake ikawa ni kutafuta fedha kwa ajili ya chakula, mavazi na matibabu. Alimaliza kidato cha sita kwa tabu kwani alilazimika kuzingatia masomo na wakati huo huo kutafuta mahitaji yao.
Lakini Mungu si Athumani, alimaliza masomo yake na matokeo yalipotoka alikuwa amefaulu vizuri kiasi cha kuwa na sifa za kupata mkopo wa elimu ya juu uliomwezesha kuhitimu na kupata shahada ya uchumi na kufanikiwa kupata kazi katika shirika fulani. Hiyo ikaleta ahueni kwao kwani aliweza kuwasomesha wadogo zake hadi chuo na hatimaye wakapata kazi na hata kuolewa. Kila mmoja wao ameolewa na anaishi kwake. Mungu mkubwa.
Sasa tatizo kubwa lililomfanya anipigie simu usiku huo ni kwamba, mwaka jana, mwanae alifanya mtihani wa darasa la saba na majibu yalipotoka alikuwa amefaulu na alipangiwa shule katika Mkoa mmoja ambao mdogo wake anayemfuata yeye ndio alikuwa akiishi na mumewe hivyo mtoto wake huyo ambaye alikuwa ni wa kike alikwenda kuishi nyumbani kwa mama yake mdogo kwani hakuona sababu ya kumpeleka shule ya bweni wakati mdogo wake yupo na yeye na mumewe wamejenga nyumba kubwa tu. Lakini pia, alitaka mwanae awe chini ya uangalizi wa mtu anayeeleweka.
Lakini tofauti na alivyotegemea yeye, mambo yalikwenda tofauti kabisa kwani mdogo wake huyo alikuwa akimnyanyasa sana mwanae huyo kwa kumpiga, kumfanyisha kazi kama punda kiasi cha mtoto kukosa muda wa kupumzika na kujisomea. Aidha, alikuwa akimsimanga na kumnyima chakula. Kila tusi lilikuwa lake. Pamoja na yote hayo, mwanae alivumilia tu na wala hakuthubutu kunieleza hata siku moja. Yote tisa, kumi ni pale alipothubutu kumpiga mwanangu hadi akazimia eti kisa ni mwanangu kwenda shule asubuhi bila ya kufagia nyumba na kuchemsha chai na kwa mujibu wa mwanae ni kwamba, siku hiyo alichelewa kuamka kwa sababu usiku alijisomea hadi saa tisa kwani alikuwa na mtihani na mchana huwa hana muda wa kujisomea. Hivyo alivyoamka alikurupuka, akavaa nguo za shule na kukimbia shule kufanya mtihani. Kimbembe kiliibuka aliporudi nyumbani kwani mama yake mdogo yule alimvaa kwa matusi na maneno ya kashfa sambamba na kipigo cha Paka mwizi hadi mtoto akapoteza fahamu kwa muda kazaa. Fahamu zilipomrejea mwanae, alikoga na kulala pasipo kula na kwa kuwa, siku kama mbili zilizopita alikuwa amemtumia pesa za matumizi mwanae, basi binti yule alichukua mizigo yake na kutoroka akaenda kupanda basi kurudi nyumbani. Kwa mujibu wa maelezo ya Mariam, mtoto alifika nyumbani usiku akiwa hoi. Amechoka na hali yake ikiwa imedhoofu. Mariamu alishindwa kujizuia kwani alijikuta machozi yakimtiririka kwa uchungu na kutokuamini kwamba, mdogo wake aliyemlea yeye mwenyewe kwa kujinyima na kwa kujituma, akamsomesha, akapata kazi na hadi akamwozesha yeye mwenyewe, leo amethubutu kumnyanyasia mwanae kiasi kile. Kama hela za matumizi alikuwa anapeleka kila mwezi. Anatuma kwa mdogo wake na kwa mtoto wake lakini malipo yake ndiyo hayao.
"Bibi, kosa langu mimi kuwasomesha na kuwafikisha hapo walipofika? Hivi mimi ningekuwa na roho kama yake, ningewalea bibi, kweli roho inaniuma sana". Mariamu alisema huku akilia kwa kwiki. Ilibidi nifanye kazi ya ziada kumnyamazisha na kumshauri na kumweleza kwamba, siku zote asitende wema akitegemea kwamba atarudishiwa wema. Eeh! Si wahenga walisema, tenda wema uende zako na wakasema pia, mfadhili mbuzi binadamu atakuudhi. Nashuru Mungu baada ya kumshauri binti wa watu alinielewa. Lakini nami kama mzazi, kama bibi yenu nikaona Mmmh!Ni lazima niseme nanyi kwani tabia ya wadada na wamama kunyanyasa watoto wa ndugu na waume zao ipo. Tena ipo sana. Sasa, najiuliza, hivi nyiye wadada na wamama mlio na tabia kama hii, tatizo hasa huwa ni nini?
Ni kwanini mnakuwa na roho za kinyama na za kikatili kiasi hiki? Kwanini mnamkaribisha shetani na mnakubali kuwa agent wake?Kwa kweli inaumiza sana na mimi huwa nasikitika kila ninapoona na kusikia taarifa za wanawake kunyanyasa na kutesa watoto. Mnawanyima vyakula, mnawafanyisha kazi kama Mbwa pasipo hata huruma kwanini lakini?
Haya, hapa juzijuzi mwanamke na akili zake timamu huko Mbeya kafanya ukatili kwa mtoto wa dada yake kabisa halafu mtoto mdogo wa miaka mitatu Yarabi kamfungia ndani na kumchoma kwa maji ya moto na hivi ninavyoandika makala hii, mtoto huyo aitwaye Aneth Johannes amekatwa mkono wake wa kushoto na yupo hospitali. Hebu niambie wewe Wilvina uliyetenda kitendo hicho cha kinyama umepata faida gani sasa? Umemtia kilema mtoto wa watu bureee. Faida iko wapi nakuuliza Wilvina. Mmh!hebu tuambie mtoto huyo mdogo alikufanyia kosa gani hasa ambayo malipo yake ni kuunguzwa maji ya moto na hatimaye kumfika?
Kwakweli, mimi ninapatwa na hasira sana kwa vitendo kama hivi. Na pengine niwaombe tu kwamba, mtu akija kukuomba uishi na mtoto wake iwe ni kwasababu yoyote ile, kama unaona huwezi, naomba umwambie aliyekuomba kwamba wewe huwezi kukaa na mawanae kuliko kukubali, na mtu anakupa mwanae kwa kukuamini halafu unakwenda kumtendea unyama wa aina hiyo. Nasema mkome. Tena mkome hasa. Na naiomba sana Serikali iwachukulie hatua kali sana wote wanaobainika kuwatendea watoto unyama kama ambavyo Wilvina alivyohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa alilotenda la kumchoma mtoto Aneth Johannes kwa maji ya moto ingawaje mimi naona kama bado adhabu hiyo haimtoshi kabisa. Watazoea hawa.
"Aah!Naona leo niishie hapa kwa sababu hasira zinanipanda kwelikweli kwa huu ujinga.
Bibi yenu,
Thereza