Friday, November 16, 2012

DUNIANI KUNA MAMBO
Ama kweli kua uyaone na wala hawakukosea waliosema ukistaajabu ya musa utayaona ya filauni.
Hivyo ndivyo ninavyolazimika kuianza makala yangu ya leo kutokana na mkasa ambao ninakwenda kuuelezea hapa chini.

Hapa kwetu Wilayani Urambo Mkoani Tabora, kuna mkasa wa ajabu ambao umetokea usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa ya tarehe 16 Novemba 2012. Picha kamili ilianza hivi.
Kijana mmoja aitwae Mdaki alifariki siku ya Jumanne baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.
Kwa mujibu wa vyanzo vyangu vya habari, Mdaki alianza kuugua ugonjwa wa kusikia anachomwa chomwa mwilini na kitu kama kisu hivi. Baada ya kuona hali inazidi kua mbaya, Mdaki alipelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Urambo ambapo alilazwa kwa siku kadhaa na alipimwa vipimo vyote lakini ugonjwa haukuonekana.
Vyanzo viliendelea kueleza kuwa, baada vipimo kutokuonyesha maradhi yanayomsumbua kijana huyu, wazazi waliamua kumtoa hospitalini hapa na kumpeleka katika hospitali ya Itigi kwa ajili ya kupata vipimo na matibabu zaidi. Lakini cha ajabu, huko nako vipimo havikuonyesha ugonjwa wowote hali ambayo ilizidi kuwachanganya wazazi pamoja na ndugu na jamaa wa karibu wa Mdaki. Na kadri siku zilivyozidi kwenda, ndivyo ambayo hali ya Mdaki ilivyozidi kuwa mbaya na kwakua vipimo havikuonyesha ugonjwa unaomsumbua Mdaki, bado wazazi hawakukata tamaa kwani waliamua kujipanga zaidi ili wampeleke katika hospitali ya KCMC ili kujaribu bahati yao. Lakini Mdaki alikataa kupelekwa KCMC na badala yake, alitaka arudishwe nyumbani Urambo kwanza halafu ndio safari ya kwenda KCMC ipangwe.
Basi, wazazi walisikiliza maneno ya Mdaki na kwa kuwa hali yake haikua nzuri kiasi cha kuweza kusafiri kwa basi kutoka Itigi kurudi Urambo, Baba Mdaki aliamua kukodi gari na ndipo safari ya kurudi nyumbani ikaanza.
Wakiwa njiani kurudi Urambo, Mdaki alizidiwa na kufariki dunia akiwa njiani.
Baada ya kifo cha Mdaki, Mazishi yalifanywa siku ya Jumatano katika makaburi ya Urasa Mjini Urambo.
Kimuhemuhe kilianza siku moja baada ya kuzikwa kwa Mdaki ( Siku ya Alhamisi) mida ya saa mbili usiku hivi.
Inaelezwa kuwa, babu yake Mdaki anaumwa na alikuwa amelala chumbani kwake. Wajukuu zake wadogo walikua chumbani humo mida hiyo wakiongea. Lakini ghafla, wakaona Paka mkubwa mithili ya Mbwa ametokea kwenye ukuta wa chumba hicho. Watoto hao ambao kwa umri ni wadogo, walipigwa na mshangao kuona kituko hicho. Wakiwa wangali wamepigwa na butwaa, Paka huyo alikua akijibadilisha rangi mara rangi hii, mara rangi ile. Kabla hawajafanya lolote, Paka yule alibadilika ghafla na kuwa Mdaki katika vazi la sanda.
Watoto hao waliogopa sana na kutoka nje mbio huku wakipiga kelele za Mdaki!Mdaki kama wehu na kuwashtua watu waliokuwepo katika eneo hilo la tukio. Wakiwa katika mbio hizo, mtoto mmoja kati ya wale watatu waliokuwemo ndani mle kwa babu alianguka chini na kuwa kama aliyekumbwa na maruhani. Wakati watu wanamshangaa, akadondoka wa pili, mara wa tatu na hatimaye watoto wengine tofauti na wale waliokuwemo chumbani kwa babu nao wakawa wanaanguka. Kusema ukweli hali ya hewa ilichafuka ghafla. Ikawa ni patashika, kelele mtindo mmoja na ndani ya kipindi kifupi, watu wakawa wamefurika kutoka katika kila pembe ya mji wa Urambo kujionea mauzauza hayo. Mji ulilizizima. Familia nzima ya Mzee Mwiniko ilichanganyikiwa.
Lakini penye wengi huwa hapaharibiki neno. Wataalam waliitwa wakapiga dua na hatimaye watu wakaweza kulala usiku huo.
Kulipokucha, makundi ya watu walimiminika nyumbani kwa mzee Mwiniko ili kushuhudia kwa macho yao miujiza hiyo na hasa ukizingatia kuwa, asubuhi kulikuwa na stori tofautitofauti kuhusiana na tukio hilo. Wapo waliosema wamemwona marehemu akiwa ameketi juu ya kaburi alilozikwa, mara wamemwona mtaani hali ambayo ilizua tafrani katika eneo hilo. Na ili kuhakikisha vurugu zinakwisha, polisi walifika katika eneo hilo na kuwasihi wananchi kuwa watulivu ili kuepuka uvunjifu wa amani na watu walielewa hivyo hali ikatulia.
Lakini hadi ninapoandika makala haya, shughuli ya kuondoka chini imesitishwa hadi itakapotangazwa tena.
Kutoka kwa ashleymama.com, tunaipa pole familia ya Mzee Mwiniko, ndugu jamaa na marafiki na kuwataka wawe watulivu sana katika kipindi hiki kigumu walichonacho. Hayo ni mapito tu na matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Aidha, kila linalotokea, hutokea kwa sabau. So, wamlilie sana Mungu wao ili wavuke salama katika maswaibu hayo. Nasi tunaendelea kuwaombea ili Mungu awatie nguvu.

MUNGU ALITOA, MUNGU AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE.
AMINA.
ashleymama.com.
Chaooooooooooooooo!