Jumatatu ya tarehe 26 Novemba, 2012 majira ya saa tatu na robo hivi, nikiwa nyumbani kwangu naangalia runinga, nilipata taarifa kuwa msanii maarufu wa vichekesho na muziki Hussein Ramadhan almaarufu kama Sharo Millionea amefariki dunia kwa ajali ya gari. Kusema ukweli, sikuamini kabisa kile nilichokisikia. Kadri muda ulivyozidi kwenda, ndivyo ambavyo meseji zinazohusu kifo cha msanii huyu zilivyozidi kumiminika katika simu yangu. Nililazimika kuingia mtandaoni na kutafuta ukweli wa jambo hili ndipo nilikutana na taarifa za kuwa kweli msanii huyu amefariki katika mtandao mmoja wa kijamii. Moyo wangu uliruka, kichwa kikanivimba, nikahisi mwili wangu kuishiwa nguvu.
"Ni nini?". Ndilo swali ambalo nilijiuliza mwenyewe na nikashindwa kujipatia jibu. Kwa sekunde kadhaa, nikajikuta nakumbuka matukio ya vifo vya wasanii kadhaa ambavyo vilitokea nyuma ndani ya mwaka huu na tena vingine vikipishana kwa siku chache tu. Bila kutegemea, nilijikuta nikishikwa na kwikwi na machozi kunitiririka kama maji. Mbona ni vijana wadogo ambao kila mmoja alikua na ndoto za kufika mbali?. Lakini baada ya kulia mwenyewe kwa muda, nilikumbuka neno la "KILA NAFSI ITAONJA MAUTI". Nilipokumbuka hilo, nilisema Amina kisha nikafuta machozi na kuanza kutafakari kwa kina juu ya vifo vya wasanii hawa, Kanumba, Mariam Khamis, Mlope, John Maganga na sasa Sharo Millionea. Neno kwanini?, kwanini? lilishika nafasi kichwani mwangu. Baadae nikajiulizia mwenyewe, au ni sauti ya Mungu? Ni Mungu anazungumza nasi kwa njia hii ili tukumbuke kuwa yupo?. Nilijitafakari mara mbilimbili kwa kujiuliza kuwa, hawa wenzetu wamekwenda na sisi tupo nyuma yao, je, Mwenyezi Mungu akiniita mimi Teddy leo hii, nitakwenda wapi?
Pengine niseme tu kwamba, vifo vya wapendwa wetu hawa, viwe funzo kwetu. Viwe funzo kwetu kwa maana kwamba, sisi kama binadamu tuishi tukijua kwamba, Mungu yupo na kifo hakichagui mtoto, kijana au mzee. Mungu akimpenda yeyote humchukua wakati wowote.
Ni vema sasa kila mmoja wetu atafakari mtindo wa maisha anaoishi. Tuishi maisha yanayompendeza Mungu kila mmoja kwa imani yake ili basi tutakapoitwa, tuwe tayari kwa maisha mapya tuliyoahidiwa.
Mwenyezi Mungu na azilaze roho za marehemu hawa wote mahali pema peponi, Aamina.
Sisi tuliwapenda lakini Mwenyezi Mungu amewapenda zaidi.
Ashleymama.com.