Siku chache zilizopita, kulitokea msiba mtaani kwetu. Kuna Bi Mkubwa mmoja alikuwa amefariki hivyo kama ilivyo ada, ndugu, jamaa, majirani na marafiki tulikusanyika kwa ajili ya mazishi ya mwenzetu huyu aliyetutoka. Siku hiyo niliomba ruhusa kazini mapema ili niweze kwenda mazishini. Eeh!Kazi zipo lakini kuhudhuria shughuli za kijamii napo ni muhimu. Kwa sababu wapo baadhi ya watu ambao wao ni wazito sana kuhudhuria shughuli za kijamii kwa kisingizio cha kubanwa na majukumu ya kazi. Kweli jamani? Hapana, mimi bibi yenu sikubaliani kabisa na suala hili na dawa ya watu hawa ipo jikoni. Ipo siku yao ya kuwacharaza bakora. Tena nitawacharaza hasa. Unamchezea bibi thereza wewe. Mimi ndie kiboko cha wale woooote walioshindikana na kujifanya majuha hawaelewi la mwadhini wala la mnadi swala. Mi nakupa tu. Ukinuna usinune shauri yako. Utajaza mwenyewe.
Haya, turudi kwenye mada yetu ya leo, basi tukiwa msibani pale, katikati ya sala ya kumwombea marehemu maana Bi Mkubwa aliyefariki alikuwa ni Mkristo, watu tukiwa tumetulia tuli tukisikiliza neno kutoka kwa mchungaji, ghafla bin vuu tukasikia kelele na zogo kutoka katika nyumba moja jirani kabisa na nyumba iliyokuwa na msiba. Zogo lilikuwa kubwa hivyo baadhi ya watu waliinuka na kwenda kwenye nyumba ile ili kuona kulikoni? Mimi bibi yenu thereza nilikuwa mmoja wa watu wale. Lakini wajukuu zangu nilipofika eneo la nyumba ile, nilipigwa na butwaa na mdomo wangu ukabaki wazi kwa mshangao baada ya kuona kituko kilichokuwepo mbele ya macho yangu. Ama kweli ukistaajabu ya Mussa, utayaona ya Filauni. Wajukuu zangu, walikuwa ni mtu na mke wake wakipigana na kutukanana matusi makubwa makubwa ya nguoni na walikuwa wamelewa chakari.
Mwanamke alikuwa amevuliwa nguo zote na kubaki na skin tight tu. Juu hana nguo hata moja. Haya, mwanaume nae, alikuwa na suruali tu, juu kifua wazi. Looh!Aibu ilioje. Watu nao ndio walikuwa wakishangilia vibaya hasa watoto. Kwa kweli bibi yenu nilibaki nimeduwaa tu na mkono wangu ukiwa shavuni.
"Hivi jamani, hawa ni watu wazima wenye akili zao timamu. Wana watoto wakubwa tu na Wajukuu, hivi kwanini wanajidhalilisha kiasi hiki na tena, wamewezaje kwenda kunywa pombe badala ya kuhudhuria msiba wa jirani yao. Haya, basi wanywe halafu waingie nyumbani kwao wakajifungia kimya. Matokeo yake wanaenda kuzua dhahama ya kuwadhalilisha kiasi hiki. Wangekuwa ni vijana wadogo tungesema ni watoto, lakini wao wazee wazima na mvi zimewajaa tele hadi kwenye kope.
Basi nikiwa nayatafakari haya, mara nikasikia kelele za kaua!Kaua!Kaua!Kaua! Umati wa watu ulikuwa ukipayuka. Mara nikaona Mwanaume aliyekuwa akimpiga mkewe akitimka mbio huku vijana wakimfukuza. Nilijisogeza karibu ili nimwone mwanamke aliyekuwa akipigwa, nilimwona akiwa amelala chini chali tuli huku damu zikimtoka mdomoni.
"Mungu wangu, huyu mama kafa jamani". Nilijikuta nikijisemea peke yangu. Mwili ulinitetemeka kweli. Baadhi ya watu walisogea karibu kumwangalia ndipo wakagundua kuwa hakuwa amekufa ila alikuwa amepoteza fahamu na meno ya juu mawili yalikuwa yametoka. Basi wamama wakamsitiri kwa kumfunika khanga na kumpepea kwa kutumia khanga ili fahamu ziweze kumrudia.
Kusema ukweli wajukuu zangu, nilikerwa mno na kitendo kilichofanywa na wanandoa hawa. Kwenda kuzusha ugomvi mchana kweupee ilihali wakijua kuwa jirani kuna msiba, jee huu ni uungwana kweli? Mtu una akili timamu utakwenda kunywa pombe wakati nyumba iliyopo mbele yako ina msiba? Haya, kunywa basi halafu ingia nyumbani kwako ulale, unaenda kuzusha ugomvi ambao unawafanya muwe sinema kwa watu.
Halafu, hayo mapenzi ni ya aina gani ya kuwa mnapigana kiasi cha kuumizana kiasi hicho? Haya, umempiga mkeo hadi umemng'oa meno kesho unampeleka mwenyewe hospitali kumhudumia hasara ya nani? Tena ni bahati katoka meno, hivi ni vipi akitoka roho? Mkono wa Serikali utakuponyesha wewe? Acheni tabia hizo bwana. Mapenzi ya kupigana ni ya kizamani sana. Mtakuja uana bure halafu muwaachie ndugu na jamaa zenu tabu. Kama mnaona mmechokana au mmeshindwana ni bora muachane. Na tena, kama pombe hamziwezi, ni bora mziache. Mbona wapo watu wanakunywa kreti nzima ya pombe lakini hawafanyi vituko vya ajabuajabu. Na nyie mkifanya hivyo, watoto na wajukuu zenu wafanyeje sasa.
Nasema vitendo vya wapenzi kupigana huwa vinanikera sana kwahiyo nawaambia mkome tabia ya kuwa mnapigana na kuvuana nguo na kupeana matusi makubwa makubwa ya nguoni halafu kesho mnalala tena kitanda kimoja. Nasema wote mlio na tabia hii muiache mara moja.
Ni mimi bibi yenu,
Thereza.
No comments:
Post a Comment