Ilikua miezi, ikawa masaa na sasa tunahesabu dakika chache tu ili kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2013. Ni wazi kwamba, kila mmoja wetu anausubiri kwa hamu mwaka mpya. Wengi wameandaa mavazi mapya, chakula na vinywaji kwa ajili ya kusherehekea siku hii kuu. Hata mimi bibi yenu usiku huu nimejilaza kwenye kochi sebuleni nikihesabu dakika moja baada ya nyingine kufikia mwaka mpya. Babu yenu naye yupo pembeni yangu. Tunaangalia luninga huku tukisubiri kuona namna mabadiliko ya teknolojia yanavyotokea. "Eeh!Si tumeambiwa tunahama sijui kutoka katika mfumo wa anolojia na kuingia katika mfumo wa digitali. Aah!Haya bwana. Ndio mambo ya maendeleo haya.
Nikiwa katika kusubiria mwaka mpya, nimeona si vyema kuukaribisha mwaka bila ya kusema nanyi wajukuu zangu. Ama kwa hakika nitakuwa sijawatendea haki hata kidogo. Taratibu nilijiinua kwenye kochi na kumwacha babu yenu, nikaelekea mezani na kuketi.Nikavaa miwani na kisha Nikachukua kalamu na karatasi na kuanza kuandika.
Wapendwa Wajukuu zangu,
Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima hadi leo hii ninaposhika kalamu na kuongea nanyi. Ee Mungu baba nasema asante kwa kuniwezesha kuifikia dakika hii. Ni wengi wameshindwa kufikia. Wapo watoto wetu, wazazi wetu, ndugu zetu, marafiki zetu na majirani zetu ambao tuliwapenda sana lakini leo hatunao kwani Mwenyezi Mungu aliwapenda zaidi. Lakini pia, wapo jamaa zetu ambao wako hoi vitandani wakipigania uhai wao. Maradhi yamewalaza vitandani ambao nao wangependa kuushuhudia mwaka huu mpya ukiingia lakini wapi kwa jinsi hii nina kila sababu ya kumshukuru Allah! kwa kunijalia pumzi hii.
Baada ya kusema hayo, hebu sasa niingie kwenye mada ambayo nataka nizungumze nanyi leo.
Kama nilivyoeleza hapo awali, tunauaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013. Jambo la muhimu la msingi ni la kila mmoja wetu kujiuliza katika kipindi kizima cha mwaka 2012, amefanya jambo gani kwake mwenye binafsi, kwa familia yake, kwa jamii inayomzunguka na Taifa zima kwa ujumla.
Ni wakati wa kujipima ili kuweza kuona ni kwa jinsi gani umeweza kutekeleza mipango yako uliyokuwa umejipangia kuitekeleza katika kipindi kizima cha mwaka 2012. Hebu jiulize, umetekeleza mipango hiyo kwa asilimia ngapi na umeshindwa kwa asilimia ngapi? Na kama umeshindwa, ni sababu zipi ambazo zimekukwamisha. Na je, umeweka mikakati ipi ili kuhakikisha kwamba, unatekeleza malengo uliyoshindwa kuyatekeleza katika kipindi hicho sambamba na kujiwekea mipango mingine mipya kwa msimu wa 2013.
Wajukuu zangu, kila kitu kinakwenda kwa mipango. Binadamu unatakiwa uweke mipango sio unaishi ishi tu ilimradi siku ziende. Ni lazima uwe na plan bwana. Kwamba kwa mwaka huu nitaanza na hili, kisha litafuata hili na baadae lile. Kama wewe huwa hujiwekei mipango, hebu anza katika mwaka huu wa 2013 ili Mungu akitujaalia uzima wa kuweza kumaliza mwaka huu, basi uweze kujipima wapi umeweza na wapi umeshindwa. Sababu zipi zimekufanya ushindwe na nini ufanye basi ili uweze kushinda.
Mimi bibi yenu ninaishi kwa mipango. Kwa mfano, katika msimu wa 2012, nilijipangia kununua kijiji nje kidogo ya maeneo ninayoishi kama maadalizi ya mahali pa kwenda kuishi mara baada ya kustaafu utumishi wa umma. Nimebakiza miaka miwili tu kustaafu. Na kwa kuwa napenda masuala ya kilimo na mifugo, nimeona nitafute Kijiji ili nitakapostaafu nikalime na kufuga kwa amani. Si mnajua tena wajukuu zangu, kufuga mjini ni kujitia pressure ya moyo tu. Maana kesi ni kila siku, mara ooh!Mifugo yako imekula mchicha wangu, mara imekula mahindi yangu, aka!Mie sitaki maneno na watu ndio maana nikaona nijinunulie kijiji.
Kwahiyo nimenunua kijiji na kujenga kajumba kangu kakupumzikia. Kazi iliyobakia ni ya kujenga banda la mifugo yangu pamoja na wigo wa nyumba yangu na hii ni mipango ambayo nimeipanga kuitekeleza katika mwaka unaokuja wa 2013.
Ninachotaka kusisitiza kwenu ni kwamba, wajukuu zangu ishini kwa mipango.Mipango ndiyo dira ya maisha yenu. Aidha, nawakumbusha pia mkumbuke ndugu zetu ambao wapo katika uhitaji( Wajane, Yatima, walemavu ) na wenzetu wengine walio katika mahitaji. Naomba sana kila mmoja kwa kadri alivyoajaaliwa, awakumbuke watu hawa. Kumbukeni kwamba, KUTOA NI MOYO SI UTAJIRI.
Mwisho, nawatakieni heri ya mwaka mpya ninyi na familia zenu. Nawaombeni sana tuupokeeni kwa amani na si kwa vurugu.
Ni mimi bibi yenu,
Thereza.
No comments:
Post a Comment