Wednesday, January 30, 2013

SIPENDI TABIA YA WANAWAKE WASIOJALI KUSAFISHA MAZINGIRA YA NYUMBA ZAO NA MIILI YAO.

Habari Wajukuu zangu. Leo nataka nizungumze na Wajukuu zangu wa kike kuhusiana na masuala ya usafi wa nyumba zao pamoja na miili yao. Ndiyo, ipo haja ya kufanya hivyo baada ya kutokuridhishwa na mazingira ya mjukuu wangu mmoja ambaye nilibahatika kufika nyumbani kwake jumamosi moja.
Siku moja nilikua katika pilikapilika za hapa na pale maeneo ya mjini. Kwa bahati nzuri, nikiwa katika pilikapilika hizo, nikakutana na mjukuu wangu mmoja ambaye anazaliwa na mtoto wa binamu yangu kabisaa. Na tulikuwa hatujaonana miaka mingi na kumbe alikuwa amehamishiwa kikazi mwezi mmoja uliopita katika mji wetu. Sasa kwa furaha aliyokuwa nayo, mjukuu wangu huyo alinichukua kwenye gari yake na kunipeleka nyumbani kwake walao nikapaone tu halafu siku nyingine ndio nitakwenda kumtembelea rasmi nikiwa na babu yenu. Pia alisisitiza niende ili pia nikamwone mke wake kwani nilikuwa sijawahi kumwona kwa sababu sikuweza kuhudhuria harusi yao kwani nilikuwa na matatizo nyumbani. Lakini pia, alikuwa na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja sasa.
Hatukuchukua muda mrefu tukawa tumefika nyumbani kwake kwani hapakuwa mbali sana na mahali tulipokuwa tumekutana. Nyumba anayokaa ni nzuri tu ya kisasa kwa mwonekano wa nje ilikuwa inaonekana ni nzuri na inapendeza. Nilishuka ndani ya gari lile na mwenyeji wangu akaniongoza hadi ndani. Tukafika sebuleni akanikaribisha na kuniacha sebuleni hapo yeye akaingia ndani kwenda kumwita mkewe. Nikiwa sebuleni hapo, nilibaki nastaajabu kwa hali ya mazingira niliyoyakuta sebuleni mle. Wajukuu zangu, kweli sebule ile ilikuwa na vitu vya thamani ya hali ya juu. Lakini mweeee!Mmh!Jamani, yaani sebule ilikuwa shaghala baghala.Haieleweki.Cha huku kimekaa kule cha kule kimekaa huku. Mara pampers za mtoto na kiatu  ziko kwenye sofa. Yaani kweli hawakukosea waliosema penye miti mingi hapana wajenzi.
Basi nikingali natafakari haya, mara mjukuu wangu anaingia akiwa amebeba mtoto wake na mkewe akimfuatia kwa nyuma. Alifika na kunikabidhi mtoto.
"Bibi, huyu ndie mwanao na huyu ndie mke mwenzio anaitwa AnnaMaria. Mjukuu wangu alinitambulisha.
"Shikamoo bibi". Aliniamkia yule mkewe.Niliitikia salamu ile. Yaani jamani, yule dada ni mzuri lakini yupo rafu saa sita ile lakini alikuwa amejifunga khanga tu, nywele zipo zipo naona hazijachanwa tangu aamke. Kwakweli nilisikitika sana maana nikimwangalia mjukuu wangu alivyokuwa akijipenda kabla hajaoa, alikuwa ni msafi, we bwana acha. Kwa kweli huyu mwanamke alinichefua sana. Hivi kweli mwanamke unashindwa kuipamba nyumba yako ikapendeza?Mtu mumewe amekuwekea kila kitu cha kisasa lakini wewe aku, huna habari? Mwanamke ukiamka nyumbani kwako kitu cha kwanza ni kufanya usafi wa nyumba yako pamoja na mwili wako. Nikiwa katika hali hiyo, mama yule alienda kwenye friji kuniletea soda kisha akaendea glasi akafungua soda na kuimimina katika glasi ile. Aah!Glasi yenyewe ilikuwa ipo ipo tu. Basi mimi nilichefukwa kweli. Kwakweli sikutaka kuendelea kukaa zaidi mahali pale, niliamua kuaga na kuondoka huku nikijiapiza kwamba, ni lazima nikawacharaze wajukuu zangu  wenye tabia za uvivu kama yeye. Eeh!Mwanaume anajinyima ananunua vitu vya thamani ili kupendezesha nyumba yake lakini wewe mwanamke unashindwa kutimiza wajibu wako, kwanini lakini. Hao masomo zenu huwa wanawafundisha nini sasa kwenye hiyo mikole yenu? Nasema mwache tabia hiyo, na mkiendelea ntaanza kuwa nawataja kwa majina ili wenzenu wawajue.
Kwa leo naishia hapa,
Ni mimi bibi yenu,
Thereza.
 

No comments:

Post a Comment